Header Ads

MABADILIKO YA DUNIA KIBIASHARA NA AJIRA



Mabadiliko ya dunia. 
                                 Karibu rafiki yangu kwenye makala yetu ya leo ambapo tutakwenda kujadili kwa kina kuhusu mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani. Ni ukweli ulio wazi kwamba dunia inabadilika, na inabadilika kwa kasi kubwa mno. 

Tukiangalia miaka kumi iliyopita, vitu vyote ambavyo tunatumia kwa sasa, havikuwepo au kama vilikuwepo basi havikuwa maarufu kama sasa. Miaka kumi iliyopita, mitandao ya kijamii tunayotumia na kufurahia sasa haikuwepo au kama ilikuwepo basi ilikuwa michanga sana. 

Miaka kumi iliyopita gharama za kupata simu zilikuwa juu kuliko ilivyo sasa, na hakukuwa na kitu kinaitwa ‘smartphone’. 
Miaka kumi iliyopita, ungeweza kuwahesabu watu wanaomiliki kompyuta au simu, lakini leo hii watu wengi zaidi wanamiliki vifaa hivi. Hakika dunia inabadilika kwa kasi kubwa sana. 

SOMA; Mabadiliko; Yalikuwepo, Yapo Na Yataendelea Kuwepo. 

Mabadiliko ya biashara. 
Biashara nazo zinabadilika kwa kasi kubwa, tukiangalia miaka kumi iliyopita na sasa kibiashara, kuna mabadiliko makubwa mno. Miaka kumi iliyopita, ungetaka kuanzisha biashara ilikubidi uwe na mtaji mkubwa, ukodi eneo la biashara na uwepo kwenye biashara yako muda wote. Ilikuwa ukitaka kutangaza biashara yako ni lazima ujiandae kwa fedha nyingi ili uweze kupata nafasi kwenye tv, redio au gazeti. Na hata kupata mtaji wa kukuza biashara ilikuwa changamoto kubwa, taasisi zilizokuwa zinatoa huduma hiyo zilikuwa chache. 

Lakini tunapoangalia leo, miaka kumi baadaye, kuingia kwenye biashara imekuwa rahisi mno. Kumekuwa na biashara mpya ambazo huhitaji hata kufungua eneo la biashara, unaweza kuendesha biashara kubwa ukiwa nyumbani kwako, ofisi ikawa hata kitanda chako, au sehemu nyingine unayoweza kuchagua ya kufanyia kazi yako. 
Kwa sasa unaweza kutangaza biashara yako kwa maelfu ya watu bure kabisa, bila kulipa gharama yoyote. Pia unaweza kutengeneza mahusiano bora na wateja wako kupitia biashara yako. 

Kitu muhimu zaidi, kwa sasa ukitaka kupata mtaji wa kibiashara, ni rahisi kuliko miaka kumi iliyopita. Sasa hivi kama unazo sifa za kupata mkopo, utafuatwa na taasisi za mikopo wakikuomba wakukopeshe, watakuambia unakopesheka na kukupa sababu nyingi kwa nini uchukue mkopo wao. Mambo yamebadilika mno katika miaka hii kumi. 

Mabadiliko ya kazi. 
Sehemu ambayo imepata mabadiliko makubwa mno ni kazi au ajira. Miaka kumi iliyopita na kurudi nyuma, wimbo maarufu ulikuwa ni huu; nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri mitihani yako, nenda chuo kikuu(au vyuo vingine), somea utaalamu fulani, ukihitimu utapata ajira nzuri na kuwa na maisha mazuri. Ilikuwa ni njia ya uhakika ambayo watu waliifuata na kuwa na maisha yanayotabirika, kwamba kama utasoma na kufaulu, una uhakika wa kuwa na kazi. Lakini tunapoangalia leo, njia hii haipo tena, wengi wamesoma na kufaulu vizuri lakini kazi hakuna. 

Hata wale ambao wapo kwenye ajira tayari, mabadiliko ni makubwa mno, miaka kumi iliyopita mtu alikazana sana apate kazi serikalini kwani ilikuwa ni uhakika wa kazi mpaka unastaafu. Lakini sasa hivi hakuna mwenye uhakika wa kazi, hata serikalini, tumeshuhudia watu wengi wakipoteza kazi zao. 

Njia za kuajiri nazo zimebadilika sana, zamani vilitumika vyeti kuajiri, aliyesoma na kufaulu vizuri alikuwa na uhakika wa kuajiriwa kutokana na vyeti vyake. Lakini sasa hivi kila mtu ana vyeti hivyo, sasa waajiri wanatafuta sifa za ziada ndiyo waweze kumwajiri mtu. 

Ni kitu gani kimebadili yote haya? 
Swali muhimu kujiuliza ni je mabadiliko haya makubwa yanayoendelea duniani, chanzo chake ni nini? Ni nguvu gani ipo nyuma ya mabadiliko haya makubwa? 
Jibu ni moja, ukuaji wa teknolojia na uwepo wa mtandao wa intaneti. Mtandao wa intaneti pekee umeleta mabadiliko makubwa mno kwenye maisha, kazi na hata biashara. 

Mabadiliko haya yataendelea kuwepo kwa sababu teknolojia bado inakuwa, na mtandao wa intaneti ndiyo kwanza unaongezeka kasi na gharama zake zinapungua. Kila siku watu wengi zaidi wanaweza kutumia mtandao huu wa intaneti. 

Mabadiliko yako wewe. 
Baada ya kuona mabadiliko yote haya, swali ni je wewe unabadilikaje? Je unabadilika au umeendelea kung’ang’ania yale ambayo yameshapitwa na wakati? Je unasubiri mpaka uwe na mtaji mkubwa ndiyo uanze biashara? Au unasubiri mpaka watu wakuone umesoma ndiyo wakuajiri? 

Vipi kuhusu kipato chako, je kinakutosha? Kama hakikutoshi ni hatua zipi umechukua ili kukiongeza? 
Kuna maswali mengi mno ninayoweza kukuuliza rafiki, lakini kitu cha muhimu nataka kukuambia hapa ni kwamba unatakiwa kubadilika. Unahitaji kuchukua hatua ili uweze kunufaika na mabadiliko haya yanayoendelea duniani. Usiishie kuwa mtazamaji na usikubali kuburuzwa na mabadiliko haya, badala yake wewe unahitaji kuwa kinara wa mabadiliko, uweze kwenda nayo sambamba. 

Unawezaje kuwa kinara wa mabadiliko na kunufaika na mabadiliko haya? 
Kuna njia moja ambayo namshauri kila mtu aitumie ili kuweza kuwa kinara wa mabadiliko. Njia hiyo ni matumizi sahihi ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Kama tulivyoona, nguvu kubwa ya mabadiliko inatokana na ukuaji wa teknolojia na mtandao wa intaneti, sasa unawezaje kuingia kwenye mabadiliko haya? 

Njia ni rahisi, unaanza kwa kuwa na blog yako ambayo utaitumia kulitengeneza jina lako na/au biashara yako. kwa kuwa watu wengi wanatumia mtandao wa intaneti kama sehemu yao ya kupata taarifa, wanapokuwa na shida au hitaji lolote, basi wanaanza kutafuta kwenye mtandao wa intaneti. Hivyo unapokuwa kwenye mtandao huu, unatengeneza njia rahisi ya watu kukufikia kwa kile unachofanya. 

Kama unafanya biashara, unaweza kuielezea na kuitangaza biashara yako kupitia blog yako. 

Kama umeajiriwa unaweza kujitengeneza na kujitangaza kama mtaalamu wa ule ujuzi ambao umeajiriwa nao, na ukatumia nafasi hiyo kutoa huduma kama za ushauri kwa wenye uhitaji. 

Kama ni msanii unaweza kutumia blog kuwasiliana na hadhira yako, pia kuwapa huduma zako. 

Kama ni mwanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu unaweza kuitumia blog kama sehemu ya kujifunza, yaani kile unachojifunza, unaweza kuwashirikisha wengine kupitia blog yako.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.